Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Cereals and Other Produce Board – CPB) ilianzishwa kwa Sheria ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Na. 19 ya mwaka 2009.Tofauti na Bodi nyingine za mazao ambazo huwa na jukumu la kusimamia zao/ mazao, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imepewa jukumu la kufanya biashara ya nafaka na mazao mengine ili kumwezesha mkulima kupata soko la uhakika na bei shindani ya mazao yake. Vilevile, Bodi ina jukumu la uendelezaji katika sekta ya nafaka na mazao mengine kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. CPB imekuwa taasisi mbadala iliyoanzishwa baada ya kufa kwa Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) na iliyokuwa Bodi ya kuuza mazao ya kilimo nje ya nchi (GAPEX). Kufa kwa taasisi hizi mbili ambazo zilikuwa zinamilikiwa na Serikali kulipelekea mkulima kukosa masoko ya uhakika. Hii ilisababishwa na kufa kwa viwanda vingi vilivyokuwa vinamilikiwa na NMC, na pia kutokuwepo chombo mahususi cha kutafuta masoko ya mazao ya nafaka na mazao mchanganyiko. Ili kuhakikisha mkulima analindwa na kuleta  uwiano sawa katika sekta ya nafaka na mazao mengine, Serikali ilianzisha Bodi hii kwa Sheria Na. 19 ya mwaka 2009. Milki za NMC ambazo zilikuwa hazijabinafsishwa hadi kufikia mwaka 2009 zimekabidhiwa kwa CPB kwa ajili ya kuziendeleza. Milki hizo ni pamoja na viwanda, ghala,vihenge na ardhi. Makao makuu ya Bodi yapo Dodoma eneo la Mbugani karibu na Bunge la Jmhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sasa Bodi inaendesha shughuli zake katika kanda tano (5)  ambazo zimegawanyika kama: Kanda ya kati (Dodoma, Singinda, Tabora, Kigoma na Katavi), Kanda ya ziwa (Mwanza, Shinyanga, Mara, Kagera,Geita na Simiyu), Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Mtwara na Lindi), Kanda ya nyanda za juu kusini (Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa na Ruvuma) na Kanda ya Kaskazini (Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga).