Majukumu ya Bodi yamegawanyika katika sehemu kuu mbili kama yalivyotajwa kwenye kifungu Na. 6 & 7 cha Sheria ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Na. 19 ya mwaka 2009. Majukumu hayo ni kama ifuatavyo:

  • Kufanya biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko
  • Kuongeza na kuendeleza thamani ya nafaka na mazao mchanganyiko

Majukumu ya kibiashara ya Bodi yanakusudia kuunda na kudhamini masoko ya uhakika ya nafaka na mazao mchanganyiko. Majukumu haya  yanahusisha shughuli za lililokuwa shirika la uuzaji bidhaa za kilimo nje ya nchi (GAPEX) ambazo ni pamoja na:

  • Kununua na kuuza nafaka na mazao mchanganyiko kwa bei shindani.
  • Kuagiza nafaka na mazao mengine kutoka nje ya nchi pale panapokuwa na upungufu wa chakula ndani ya nchi.
  • Kuuza nafaka na mazao mchanganyiko nje ya nchi. 

Majukumu ya uendelezaji na uongezaji thamani ya Bodi hushirikiwa na wadau wengine katika tasnia ya nafaka na mazao mengine. Majukumu haya yanahusisha shughuli za lililokuwa Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) ambazo ni pamoja na:

  • Kutoa huduma za ghala za kuhifadhi nafaka na mazao mchanganyiko, kutoa usafishaji, ukaushaji, upimaji, upangaji madaraja na ufungashaji wa nafaka na mazao mchanganyiko kulingana na viwango vya soko.
  • Kuongeza thamani nafaka na mazao mchanganyiko kupitia uchakataji wa viwanda.

 Majukumu mengine ya pamoja kwa kushirikiana na wadau wengine ni pamoja na;

  • Kufanya tafiti za kilimo katika sekta ya nafaka na mazao mchanganyiko.
  • Kutoa huduma za ugani kwa wakulima wa nafaka na mazao mchanganyiko.
  • Kuwezesha upatikanaji wa huduma za pembejeo (mbegu, mbolea na viuwatilifu).
  • Kukuza uzalishaji, masoko, usindikaji na uhifadhi wa nafaka na bidhaa nyingine.
  • Kushiriki katika utoaji wa taarifa katika tasnia ya nafaka na mazao mchanganyiko.
  • Kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya tasnia ya nafaka na mazao mchanganyiko.
  • Kushiriki katika utoaji ushauri kwa vyama vya wakulima au vyama vya ushirika.